Want to partner with us? Let's get started now!

Kongamano la kitaifa la Wanaushirika kwa mwaka 2019, Jijini Mbeya

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhuisha na kuujenga upya ushirika kwa kufanya mapitio ya Sera ya Ushirika na Sheria zake na kuwahusisha kikamilifu wadau wa Sekta hiyo katika kutoa maoni.

Dkt. Kamani ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la kitaifa la Wanaushirika lililofanyika leo 05 Jul 2019 jijini Mbeya na kuhudhuriwa na viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika nchini ambapo amewataka kutoa maoni yao kwenye maboresho yanayofanywa na Serikali katika Sekta ya Ushirika.

“Tumieni majukwaa haya vizuri kwa kutoa maoni yenye lengo la kujenga Sekta hii muhimu kwa uchumi wa wananchi na wa Taifa kwa ujumla; tumieni mtandao mkubwa ulioko katika Sekta ya Ushirika ili kuimarisha nguvu yenu katika kutafuta masoko ya mazao yenu,” alisema Dkt. Kamani.

Aidha, Dkt. Kamani amewataka Watendaji wanaoajiriwa katika vyama vya ushirika kuwa waadilifu na kufuata miiko ya kazi zao ili kutimiza malengo ya wanachama wa vyama hivyo wakati wa kuanzishwa.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Bwana Tito Haule, amewataka Watendaji katika vyama vya ushirika kuacha kujichukulia wajibu wa kufanya maamuzi makubwa katika vyama hivyo; na badala yake maamuzi hayo yafanywe na Bodi za vyama husika, ambao wamekabidhiwa mamlaka hayo na wanachama wao.https://www.ushirika.go.tz/news/simamieni-vyama-vya-ushirika-kwa-ufanisi-zaidi-dkt-kamani/1

“Baadhi ya Watendaji wana nguvu kubwa kuliko hata Bodi zao, hii siyo sahihi, maamuzi makubwa katika chama cha ushirika lazima yafanywe na Bodi, ambao ndiyo waliokabidhiwa kusimamia mali za wanachama kwa niaba yao,” alisema Mrajis.

Akizungumzia kuhusu mapitio ya Sera ya Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Bwana Tito Haule, amewaomba wadau wa ushirika kuandika na kuwasilisha maoni yao kwa kile wanachoona kinafaa kujumuishwa kwenye Sera mpya itakayokuja.

Katika kongamano hilo la wanaushirika, wajumbe pamoja na mambo mengine walijadili na kutoa maoni yao kwenye mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002 ili kukidhi mazingira ya sasa katika Sekta ya Ushirika.

Tume ya Maendeleo ya Ushirika imetakiwa kuendelea kuhamasisha wananchi wengi kujiunga na Vyama vya Ushirika kwa kuwa kuna manufaa mengi zaidi ambayo mwananchi anayapata.

Wito huo umetolewa leo tarehe 06 Jul 2019 na Mheshimiwa Kassimu Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Omari Mgumba (Mb), kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya.

“Tuendelee kuwahamasisha wananchi wetu kujiunga katika Vyama vya Ushirika kwani kupitia Vyama vya Ushirika kuna manufaa makubwa ambayo mwananchi anayapata. Hivyo, tuhakikishe ifikapo mwishoni mwa mwaka huu angalau idadi ya wanachama ifikie milioni sita,” alisema Waziri Mkuu.

Aidha, Waziri Mkuu ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinafanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara; kuanzishwe SACCOS katika maeneo yaliyo na AMCOS; kuhakikisha mazao yanayolimwa na wakulima yanaendelea kupata masoko ya uhakika kwa kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali.

Hadi kufikia mwezi Februari, mwaka 2019, nchi yetu ina jumla ya Vyama vya Ushirika 11,331 vyenye idadi ya wanachama 3,998,193 nawanachama tarajiwa 1,378,882, idadi hii imeongezeka kutoka Vyama vya Ushirika 10,990 vyenye wanachama 2,385,295 kwa mwaka 2018. Hivyo, kwa kipindi cha mwaka mmoja vimeongezeka Vyama vya Ushirika 341 na wanachama wameongezeka 1,612,898.

Wanachama wa Vyama vya Ushirika nchini wameweza kuanzisha shughuli za maendeleo kama vile: bustani, ufugaji na biashara za aina mbalimali ili kujipatia fedha za kujikimu katika maisha ya kila siku, kununua vyombo vya usafiri, kugharamia matibabu, kujenga nyumba bora na kuwasomesha watoto katika ngazi mbalimbali za elimu na wengine wamefikia hadi elimu ya Chuo Kikuu kutokana na fedha ya karo, chakula na huduma nyingine kutoka Vyama vya Ushirika.

Kupitia Vyama vya Ushirika uzalishaji wa mazao mbalimbali hasa ya kimkakati umeongezeka kwa mfano katika Mkoa wa Mbeya kwa msimu wa mwaka 2017/2018 uzalishaji wa zao la Kakao ulikuwa kilo 9,980,000 lakini kwa mwaka 2018/2019 uzalishaji wa miezi minane sasa umefikia kilo 7,509,470 na bado masoko yanaendelea na matarajio ni Kilo 11,620,000 hadi mwishoni mwa msimu.

Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo vimeendelea kutoa mikopo kwa wanachama wake, mikopo ambayo imesaidia kuleta maendeleo kwa jamii kwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kufanya biashara ndogondogo.

Singo Africa Limited ambao ni wadau wakubwa wa ushirika katika sekta ya TEHAMA, waliweza kushiriki katika jukwaa hilo ipo tayari kushirikiana kutoa elimu kwenye vyama ushirika kwa ukaribu kuanzia ngazi za wanachama, viongozi, maafisa ushirika pamoja na wadau wote wa ushirika kwa ujumla katika kukuza sekta hiyo.

About the Author

Leave a Reply

You may also like these